14 Julai 2024 - 06:16
MASWALI NA MAJIBU (2) - Je, Imam Hussein (a.s) aliuawa kishahidi na Mashia?!

Wauaji wa Imam Hussein(a.s) walikuwa ni maadui zake, hivyo Mashia wa Imam Hussein(a.s) hawawezi kuwa wauaji wa Imam Hussein(a.s) kwa sababu wao ni Mashia (Wafuasi) wa Imam Hussein(a.s), na (Wafuasi) Mashia wake kamwe hawawezi kuwa maadui wa Imam wao.

Katika kujibu swali hili, tutaashiria katika nukta zifuatazo hapo chini:

Nukta ya Kwanza:

Wale watu waliokuwepo Karbala na ambao walikuwa ni miongoni mwa wauaji wa Imam Hussein(a.s), walikuwa ni vipenzi na wafuasi wa Yazid na Muawiyah, hivyo hawakuwa ni sehemu ya Mashia wa Imam Hussein(a.s).

“Kharazmi” anaandika katika kitabu kiitwacho "Maqtal al-Hussein" akinukuu maneno ya Imam Hussein (a.s):

«وَيْلَكُمْ يَا شِيعَةَ آلِ أَبِي سُفْيَانَ إِنْ لَمْ يَكُنْ لَكُمْ دِينٌ وَ كُنْتُمْ لَا تَخَافُونَ الْمَعَادَ فَكُونُوا أَحْرَاراً فِي‏ دُنْيَاكُم»

“Ole wenu enyi Mashia (Wafuasi) wa familia ya Abu Sufyan, ikiwa hamna dini na wala hamuogopi hisabu ya Siku ya Kiyama, basi angalau kuweni watu huru katika dunia yenu”. Rejea (Maqtal al-Hussein: Juzuu ya 2, Ukurasa wa 38).

(Ikumbukwe kwamba “ Kharazmi ” ni mmoja wa Wanazuoni wakubwa wa Kisunni, na Ahlu Sunna wanamchukulia kuwa ni Mwanasayansi (Aalim) mkubwa katika sayansi (ilimu) ya Historia na Sira).

Nukta ya Pili:

Kimsingi, kuna mgongano (au hali ya kukinzana) katika kauli hii kwamba “Mashia wa Imam Hussein (a.s) walimuua Imam Husein (a.s)”, kwa sababu Mashia wa Imam Hussein(a.s) maana yake ni wafuasi wake.

Wauaji wa Imam Hussein(a.s) walikuwa ni maadui zake, hivyo Mashia wa Imam Hussein(a.s) hawawezi kuwa wauaji wa Imam Hussein(a.s) kwa sababu wao ni Mashia (Wafuasi) wa Imam Hussein(a.s), na (Wafuasi) Mashia wake kamwe hawawezi kuwa maadui wa Imam wao.

Nukta ya Tatu:

Hebu tuchukulie kwamba Mashia wa Imam Hussein (a.s) ndio waliomuua Imam wao Hussein (a.s)!. Swali letu litakuwa ni hili: Je, walikuwa wapi Waislamu wengine (wasiokuwa Mashia wa Imam Hussein -a.s-) katika tukio la chungu la - kuchinjwa kinyama kwa Mjukuu wa Mtume (s.a.w.w) katika ardhi ya - Karbala?!. Kwa nini hawakujitokeza kukumtetea na kumhami Imam Hussein (a.s)?!.

Kwa hiyo, hapo ni lazima isemwe kwamba Waislamu wengine (wasio kuwa Mashia wa Imam Hussein -a.s-) ima walihusika katika kumuua Imam Hussein (mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w.w) au isemwe kwamba waliamua kunyamaza kimya katika tukio la Karbala, kwa vyovote vile katika hali zote mbili uhalifu huu bado utaandikwa na kusajiliwa kwa majina yao.

Nukta ya Nne:

Je, wale watu (maelfu ya majeshi) waliokuja katika ardhi ya Karbala kupigana vita dhidi ya Imam Hussein(a.s). walikuwa Mashia?!. Tafadhali zingatia (na tia akilini) riwaya hii ifuatayo:

·       "Al-Qunduzi Al-Hanafi" anasimulia kwamba huko Karbala, baadhi ya wauaji wa Imam Hussein (a.s) walimwambia Imam Hussein(a.s): «إنّا نَقتُلُكَ بُغضَاً لِأبيك» “Tunapigana na wewe vita kwa sababu ya chuki tuliyonayo kwa baba yako”. (Yanabi' al-Mawaddah: Juzuu ya 3, Ukurasa wa: 72).

Je, watu hawa waliopigana dhidi ya Hadhrat Sayyid al-Shuhadaa, ili wamuue kwa sababu ya chuki zao nyoyoni mwao dhidi ya Amirul-Mu'minin Ali bin Abi Talib(a.s), walikuwa ni Mashia (wa Imam Hussein -a.s-)?!

·       "Ibn Athir" anasimulia kwamba mmoja wa watu waliokuwa katika jeshi la "Umar bin Saad" alifoka akimnadi Imam Hussein (a.s) kwa kusema: «يَا حُسَيْنُ يَا كَذَّابُ ابْنَ الْكَذَّابِ!» "Ewe Hussein!, Ewe muongo mwana wa muongo!" Rejea: (Al-Kāmil fit-Tārīkh: Juzuu ya 4, Ukurasa wa: 67).

Je, watu kama hao, walikuwa miongoni mwa Mashia wa Imam Husein (a.s)?!.

·       “Ibn Athir” anasimulia kuhusu kauli ya mtu mwingine katika jeshi la “Omar bin Saad” kwamba alimwambia Hadhrat Sayyid al-Shuhadaa (a.s):   «يَا حُسَيْنُ أَبْشِرْ بِالنَّارِ!» “Ewe Hussein, karibu kwenye moto wa Jahannamu”! Rejea: (Al-Kāmil fit-Tārīkh: Juzuu ya 4, Ukurasa wa: 66). Je, mtu kama huyo anachukuliwa kuwa ni Shia wa Imam Hussein (a.s)?!.

·       "Ibn Kathir, Salafi wa Damascus" anasimulia akisema:

«وَ دَخَلَ عَلَيْهِمْ وَقْتُ الظُّهْرِ فَقَالَ الْحُسَيْنُ: مُرُوهُمْ فَلْيَكُفُّوا عَنِ الْقِتَالِ حَتَّى نُصَلِّيَ، فَقَالَ رَجُلٌ مِنْ أَهْلِ الْكُوفَةِ: إِنَّهَا لَا تُقْبَلُ مِنْكُمْ، فَقَالَ لَهُ حبيب بن مطهر: ويحك!! أتقبل منكم وَ لَا تُقْبَلُ مِنْ آلِ رَسُولِ اللَّهِ؟».

Siku ya A’shura, wakati wa sala ya adhuhuri ulipofika, Hussein akawaambia Masahaba zake: Nendeni mkawambie madui waache kupigana vita (wasimamishwe vita kwa muda wa dakika kadhaa) ili tuswali kwanza. Wakati huo, mtu mmoja ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa al-Kufa alisema akimjibu Imam Hussein (a.s): Wewe Sala yako haikubaliwi!. Habib bin Madhahir akamjibu moja kwa moja akisema: Ole wako! Je, ni kweli kwamba sala yako wewe inakubaliwa, lakini sala ya mtu wa Nyumba ya Mtume haikubaliwi?!. Rejea: (Al-Bidayah Wan Nihayah: Juzuu ya 8, Ukurasa wa: 185).

Kwa kuzingatia nukta hizi na zingine, je, bado inawezekana kuendelea kusemwa kwamba wale waliomuua Kishahidi Imam Hussein (a.s) walikuwa ni Mashia wake?!!!